Siku ya Alhamisi, Hoang Thi Minh Hong, mwanaharakati maarufu wa hali ya hewa na mfanyakazi wa zamani wa Mfuko wa Ulimwengu Pote wa Mazingira (WWF), alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela na kutozwa faini ya dola 4,100 baada ya kukutwa na hatia ya kukwepa kulipa kodi.
Kesi yake ilidumu kwa saa tatu pekee, na upatikanaji wa wakili wa familia na wa utetezi ulipunguzwa muda wote alipokuwa kizuizini.
Isitoshe, mashtaka dhidi yake yanaweza kuwa yamechochewa kisiasa, kulingana kwa wataalam huru wa haki za binadamu.
'Ukandamizaji mpana'
Anakuwa wa tano kati ya watetezi sita wa haki za binadamu wa mazingira waliokamatwa tangu 2021, kuhukumiwa.
"Watetezi wengine wanne wa haki za mazingira wamefunguliwa mashitaka kwa mashtaka sawa na kuhukumiwa kifungo cha hadi miaka mitano, katika kile kinachoonekana kuwa ukandamizaji mpana zaidi dhidi ya watetezi wa haki za mazingira na dhidi ya nafasi ya kiraia nchini Viet Nam," Msemaji Jeremy Laurence alisema.
Mashtaka yaliyotolewa dhidi ya mtu wa sita aliyesalia bado hayajawekwa wazi.
'Athari ya kutuliza'
Kukamatwa kunahitaji kutazamwa kwa kuzingatia Ushirikiano wa Mpito wa Nishati wa Viet Nam, OHCHR sema.
Ni ushirikiano wa kimataifa ulioundwa kusaidia juhudi za uondoaji wa ukaa katika mataifa yanayoendelea, na Viet Nam ilifungua Sekretarieti yake mwezi Julai, kulingana na ripoti za habari.
Ofisi hiyo ilikariri kuwa ili kufikia mafanikio ya mpito ya haki na endelevu kwa nishati ya kijani, watetezi wa haki za binadamu na mashirika ya mazingira lazima wawe na uhuru wa kushiriki kikamilifu na bila vikwazo katika kuunda sera na kufanya maamuzi.
"Mashtaka haya na matumizi ya kiholela ya sheria yenye vikwazo yana athari mbaya kwa kazi muhimu sana ya watetezi wa mazingira, na ile ya watetezi wengine wa haki za binadamu nchini Viet Nam," Bw. Lawrence alisema.
Wito wa kutolewa bila masharti
Aliitaka Serikali kuacha kutumia mashtaka ya jinai kuminya matumizi ya uhuru wa kimsingi na kuwaachilia bila masharti wale wote ambao wameshikiliwa katika kesi hizo.
"Pia tunakumbusha mamlaka juu ya wajibu wao chini ya sheria ya kimataifa ya kuheshimu utawala wa sheria, haki ya kesi ya haki, na kuhakikisha uhuru wa mahakama."