Mlipuko wa siku ya Jumatatu - karibu na mpaka wa Uturuki - ulilenga gari lililokuwa likisafirisha wafanyikazi wa kilimo wa msimu. Kulingana na ripoti za habari, wanawake wasiopungua 11 na watoto watatu walikuwa miongoni mwa waliofariki.
Inafuatia shambulio lingine siku chache zilizopita lililoua raia wanne na kuwajeruhi wengine tisa, wakiwemo watoto sita. Mlipuko wa bomu uliotokea Jumatatu kwenye gari umeripotiwa kuwa wa saba katika muda wa mwezi mmoja tu na ni shambulio baya zaidi nchini Syria tangu kuanguka kwa utawala wa Assad.
Eneo hilo limekuwa uwanja wa vita kwa wanajeshi wanaoungwa mkono na Uturuki na wengi wao wakiwa ni wapiganaji wa Kikurdi. Hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulio hilo la Jumatatu hadi sasa.
"Tunasisitiza kwamba pande zote lazima zitekeleze wajibu wao chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu ili kulinda raia,” alisema Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric, akiwahutubia waandishi wa habari mjini New York.
"Raia na miundombinu ya kiraia haipaswi kulengwa kamwe."
Maelfu wameyahama makazi yao
Wakati huo huo, mapigano yanaendelea kaskazini mashariki mwa Syria, haswa mashariki mwa Aleppo, Al-Hasakeh na Ar-Raqqa, ambapo zaidi ya 25,000 wameyakimbia makazi yao.
Makombora, mashambulizi ya anga na mapigano yanayoendelea yameharibu jamii, na kusababisha uharibifu mkubwa wa nyumba, hospitali na miundombinu muhimu, kulingana na taarifa ya kibinadamu iliyotolewa na ofisi ya kuratibu misaada ya Umoja wa Mataifa. OCHA.
Kote nchini, ukosefu wa huduma za umma na ufadhili umefanya kuwa vigumu kwa mashirika ya kibinadamu kujibu.
Huko Homs na Hama, umeme unapatikana kwa dakika 45 hadi 60 pekee kila baada ya saa nane, wakati kaskazini-magharibi mwa Syria, zaidi ya vituo 100 vya afya vimekosa ufadhili tangu kuanza kwa mwaka huu.
Umoja wa Mataifa na washirika wake wanaomba dola bilioni 1.2 kusaidia watu milioni 6.7 walio hatarini zaidi nchini Syria hadi Machi 2025.
Juhudi za kibinadamu
Licha ya changamoto hizo, mashirika ya Umoja wa Mataifa na washirika wanaendelea na juhudi zao za kutoa msaada na kufuatilia hali hiyo, kadri usalama unavyoruhusu.
Mnamo Februari 3, ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuvuka mpaka kutoka Türkiye hadi Idlib ulitathmini jitihada za usambazaji wa fedha - sehemu ya jitihada pana kufikia jamii zinazohitaji.
"Hadi sasa mnamo 2025, tulikamilisha misheni 40 za kuvuka mpaka nchini Syria, nyingi zikiwa za kufuatilia na kutathmini miradi - karibu mara mbili ya idadi ya misheni tuliyokuwa nayo wakati huo huo mwaka jana," Bw. Dujarric alisema.
Mnamo Januari 30, timu za Umoja wa Mataifa pia zilifanya ujumbe wa tathmini huko Sweida, karibu na mpaka wa Jordan, kuashiria uwepo wa kwanza wa Umoja wa Mataifa katika eneo hilo tangu Oktoba 2023. Ziara hiyo ilifichua uhaba mkubwa wa maji ya kunywa na rasilimali za umwagiliaji, uliosababishwa na ukame wa miaka mingi.
Wakimbizi wanarudi
Wakati huo huo, utafiti wa hivi karibuni wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, iligundua kuwa asilimia 27 ya wakimbizi wa Syria katika Jordan, Lebanon, Iraq na Misri, wanapanga kurejea nyumbani ndani ya miezi 12 ijayo. - ongezeko kubwa kutoka chini ya asilimia 2 iliyorekodiwa Aprili mwaka jana.
Tangu kuanguka kwa utawala wa Assad mwezi Disemba, hadi Januari 23, zaidi ya Wasyria 210,000 wamerejea huku wengi wakikabiliwa na changamoto zinazohusiana na uharibifu wa mali, ukosefu wa miundombinu na masuala ya usalama.
Wakimbizi wa ndani (IDPs) ndani ya Syria pia wanaanza kurejea nyumbani, ingawa ni wachache.
Tangu mapema Desemba, takriban 57,000 IDPs - wengi wao wakiwa vikundi vya familia moja au watu binafsi - wameondoka kwenye kambi za IDP.
Walakini, karibu watu milioni mbili wamesalia katika kambi zaidi ya 1,500 kote Idlib na kaskazini mwa Aleppo, ambapo wasiwasi wa usalama na ukosefu wa huduma muhimu unaendelea kuzuia kurudi.